Feature Image

Netanyahu aagiza jeshi kuharibu ngome zote za Hezbollah

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameliagiza jeshi la nchi hiyo kuongeza mashambulizi na kuharibu miundombinu yote ya kundi la wanamgambo la Hezbollah, linaloungwa mkono na Iran, katika eneo la kusini mwa Lebanon.

Akiwa katika ziara ya kuwatembelea wanajeshi wa Israel, Netanyahu alisema agizo hilo linahusu miundombinu yote ya Hezbollah—iwe juu ya ardhi au chini ya ardhi—ikiwemo mtandao wa mahandaki ambao umekuwa ukitumika kurusha mashambulizi dhidi ya Israel.

Netanyahu amesisitiza kuwa jeshi la Israel halitaondoka katika maeneo ya mpakani hadi pale Hezbollah itakapoweka chini silaha na kutokuwa tena tishio kwa usalama wa Israel.

Kiongozi huyo amelitaja kundi hilo kama kiungo muhimu katika mtandao wa washirika wa Iran, akidai kuwa Israel imefanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa uwezo wa kijeshi wa Hezbollah.

Kwa upande mwengine, serikali ya Lebanon pamoja na Hezbollah zimepinga vikali hatua ya Israel, zikieleza kuwa eneo la usalama lililoanzishwa na Israel kusini mwa Lebanon ni uvamizi unaokiuka sheria za kimataifa.

Kwa mujibu wa makadirio ya kijiografia yaliyoripotiwa na vyombo vya habari vya Lebanon, eneo linalodhibitiwa na Israel lina ukubwa wa takriban kilomita za mraba 620, sawa na karibu asilimia 6 ya eneo lote la Lebanon.