WADAU 'WAPAGAWA' VIVUTIO BANDA LA MALIASILI SABASABA
WADAU 'WAPAGAWA' VIVUTIO BANDA LA MALIASILI SABASABA
Na Mwandishi Maalum, MNRT
WANANCHI mbalimbali wakiwemo walimu na wanafunzi wameeleza kushangazwa na vivutio vilivyo ndani ya Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa wanafunzi walioeleza kufurahishwa na vivutio ndani ya Banda la Maliasili ni wa Shule ya Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza ya Majority iliyopo Pugu jijini Dar es Salaam.
Wanafunzi David Nsolo wa darasa la sita katika shule hiyo na Mariam Nkoba wa darasa la tano wamesema wamefurahishwa na wanyamapori hai waliowaona ndani ya Banda hilo wakiwemo Chui na Duma.
"Mara zote nimekuwa namuona Chui katika televisheni lakini leo nimemuona uso kwa uso jambo ambalo limenifurahisa sana," alisema David.
Naye Mariam alisema; " Kwangu mimi hii ni mara ya pili, mwaka jana pia nilikuja na mwaka huu nimekuja tena maana napenda kuwaona wanyama ana kwa ana ni jambo linalonijengea ujasiri katika maisha yangu ya kawaida."
Walimu kutoka Shule ya Msingi Migombani wilayani Temeke, Hosea Obadia na Lwitiko Mwankenja wameeleza kuvutiwa na Utalii wa Kiutamaduni zikiwemo nyumba za asili ambazo waliishi miaka mingi iliyopita wakiwa kijijini.
"Huu ubunifu wa kuleta hii nyumba ya nyasi hapa umenivutia sana. Hiki ni kielelezo cha Uafrika wetu na nadhani wageni wengi wa kutoka nje watapenda kufika hapa," alisema Mwankenja.
Kwa upande wake Mwalimu Hosea alisema maeneo yote ndani ya Banda yanavutia akielezea pia kufurahishwa na 'goli la maajabu' la AFCON 2027 nililopo ndani ya Banda la Maliasili ambapo watoto wanapewa mipira na kucheza kama sehemu ya kuhamasisha vipaji vya watoto katika mchezo wa Soka kuelekea Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) yatakayofanyika nchini baadaye mwakani.
Ikiwa ni siku ya nne tangu kuanza kwa Maonesho ya Sabasaba, maelfu ya wakazi wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani wamekuwa wakimiminika ndani ya Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kujionea vivutio mbalimbali hususani katika tasnia ya Utalii.
Maonesho hayo ya 50 ya DITF yanatarajiwa kufunguliwa rasmi Julai 4, 2026, na kumalizika Julai 13. 2026, huku viongozi mbalimbali wa ndani na nje wakitarajiwa kuhudhuria.