Feature Image

Wajumbe wa Iran, Marekani wazungumza na wapatanishi Doha

Iran imetuma wawakilishi kwa mazungumzo na wapatanishi kwenye mazungumzo nchini Qatar kukomesha vita vilivyoanzishwa dhidi yake na Marekani na Israel lakini bila ya kukutana moja kwa moja na wenzao wa Washington.

Iran imetuma wawakilishi kwa mazungumzo na wapatanishi kwenye mazungumzo nchini Qatar kukomesha vita vilivyoanzishwa dhidi yake na Marekani na Israel lakini bila ya kukutana moja kwa moja na wenzao wa Washington.

Awali chanzo kimoja cha kidiplomasia kilicho karibu na mazungumzo hayo kilikuwa kimeliambia shirika la habari la AFP kwamba maafisa wa Marekani na Iran walipangiwa kufanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kwenye ngazi ya wataalamu siku ya Jumatano (Julai 1) mjini Doha.

"Wanakutana na wapatanishi wa Pakistan na Qatar kuzungumzia Makubaliano ya Awali na kutathmini maendeleo yaliyopatikana kwenye Mkutano wa Kilele wa Ziwa Lucerne." Kilisema chanzo hicho.

Hata hivyo, wajumbe wa Marekani, Steve Witkoff na Jared Kushner, hawakupangiwa kushiriki mazungumzo ya wataalamu, kwa mujibu wa mwanadiplomasia huyo, baada ya kwamba tayari wawili hao walishakutana na Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani siku ya Jumanne (Juni 30).

Hakuna kikao cha moja kwa moja

Iran ilikiri kuwa wawakilishi wake wangelikuwapo Doha kwa ajili ya kukutana na wapatanishi, lakini ilipinga vikali kauli ya Trump kwamba kungelikuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani. 

Msimamo huo wa Iran uliungwa mkono na Qatar, ambayo kupitia wizara yake ya mambo ya nje ilisema hakukupangwa mkutano wowote wa ngazi za juu wala mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani.

"Wawakilishi wa Marekani wapo hapa sio kwa mazungumzo yao na wa Iran. Bali kukutanana wapatanishi na maafisa wa Qatar. Mazungumzo yalijumuisha suala la Iran na pia suala la Lebanon." Msemaji wa wizara hiyo, Majid Al Ansari, aliandika kwenye mtandao wa X.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran, Esmael Baqaei, alithibitisha kuwasili kwa ujumbe wa nchi yake mjini Doha ukiongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Kazem Gharibabadi.

Israel kuendelea kuikalia Lebanon

Kwenye upande mwengine wa mzozo, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu aliliamuru jeshi lake kuiharibu kabisa miundombinu yote ya kundi la Hizbullah kusini mwa Lebanon. 

"Hii ndiyo amri yangu: Musibakishe chochote, na fanyeni hivyo." Alisema Netanyahu siku ya Jumanne (Juni 30) baada ya kuvitembelea vikosi vya jeshi lke kwenye eneo la mapambano.

Amri hiyo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa baadaye na serikali yake, inajumuisha kuyaharibu majengo ya juu na ya chini ya ardhi, yakiwemo mahandaki, ambayo yametumiwa na wanamgambo hao kuishambulia Israel. 

Hata hivyo, kwa kuzingatia kilichofanywa na Israel kwenye Ukanda wa Gaza na pia kwenye miji na vijiji vyengine vya Lebanon, wengine wanahofia kuwa amri hiyo inamaanisha kuyaangamiza kabisa makaazi ya watu kiasi cha kuyafanya yasikalike tena.

Netanyahu alirejelea msimamo wake kwamba jeshi la Israel halitaondoka kwenye maeneo lililoyateka ndani ya ardhi ya Lebanon, hadi pale wanamgambo wa Hizbullah watakapokuwa wamenyang'anywa silaha. 

Ikumbukwe kuwa kukomeshwa kwa mashambulizi na ukaliaji wa Israel ndani ya Lebanon ni mojawapo ya vipengele muhimu kwenye Makubaliano ya Awali kati ya Iran na Marekani kuelekea kukomesha vita vya Mashariki ya Kati.