Feature Image

RAIS SAMIA AMTAKA DKT. MAGEMBE KUSIMAMIA IPASAVYO SEKTA YA AFYA, VIPAUMBELE VIFIKIWE

 

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, leo Julai Mosi, 2026 amemuapisha Dkt. Grace Magembe kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, akimkabidhi jukumu la kusimamia utekelezaji wa sera, mipango na bajeti ya sekta hiyo huku akisema kuwa, uzoefu wake wa muda mrefu katika utumishi wa umma ni msingi wa imani aliyomwekea katika nafasi hiyo.

Akiongea wakati wa hafla ya kuapishwa iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam na kurushwa mbashara na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Rais Samia amesema Dkt. Magembe anakwenda kusimamia Wizara ya Afya katika kipindi ambacho Bunge limepitisha bajeti muhimu ya sekta hiyo, hivyo akamtaka kuhakikisha kila fedha inayotolewa inaleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi.

"Unakwenda kusimamia bajeti ambayo imepitishwa na Bunge. Hakikisha utekelezaji wake unaleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi na kila shilingi inatumika kwa uadilifu na kwa manufaa ya Watanzania," amesisitiza Rais Samia.

Aidha, Rais ametaka Katibu Mkuu huyo mpya kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba unaendelea kuimarika katika hospitali, vituo vya afya na zahanati nchini, akieleza kuwa wananchi wanatarajia kuona matokeo ya uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali kwenye sekta ya afya kupitia huduma bora na zinazopatikana kwa wakati.

"Wananchi wanahitaji kuona dawa zinapatikana, vifaa tiba vinakuwepo na huduma zinatolewa kwa ubora unaostahili. Hilo ni jukumu ambalo lazima lisimamiwe kwa karibu," amesema Rais Samia

Katika maelekezo yake, Rais Samia amehimiza umuhimu wa kujenga mahusiano mazuri na watumishi wa Wizara ya Afya, akimtaka Dkt. Magembe kuwa kiongozi anayesikiliza, anayeshirikisha na anayejenga timu yenye mshikamano, akiamini kuwa mafanikio ya wizara yanategemea ushirikiano wa watumishi wote.

"Nenda ukaishi vizuri na watumishi. Washirikishe, wasikilize na waongoze kwa haki, kwa sababu mafanikio ya wizara yanajengwa na timu, si mtu mmoja," amefafanua Rais Samia

Katika hatua nyingine Rais Samia pia amemhakikishia Dkt. Magembe kuwa Serikali itaendelea kumpa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake, akieleza kuwa atakuwa tayari kumshauri na kumuunga mkono pale itakapobidi ili kuhakikisha sekta ya afya inaendelea kufikia malengo ya Serikali ya kuboresha huduma kwa wananchi.

Uteuzi wa Dkt. Grace Magembe, ambaye amewahi kuhudumu katika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo Mganga Mkuu wa Serikali, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI unatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa kuimarisha utendaji wa Wizara ya Afya katika kusimamia utekelezaji wa bajeti, kuendelea kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kufikia asilimia 60 ifikapo 2030, pamoja na kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya kwa wakati.