Rais Yoweri Kaguta Museveni ameapishwa kuiongoza Uganda kwa muhula wa saba mfululizo katika sherehe kubwa zilizofanyika uwanja wa Kololo, jijini Kampala.
Rais Yoweri Museveni ameapishwa kuiongoza Uganda kwa muhula wa saba katika hafla iliyofanyika mjini Kampala.
Mkuu wa majeshi, Jenerali Muhoozi Kainerugaba - ambaye pia ni mtoto wa rais na anayetajwa kama mrithi wake - alisimamia mazoezi ya gwaride la kijeshi yaliyofanyika kwa siku kadhaa kabla ya sherehe hiyo. Ndege za kivita za Urusi aina ya Sukhoi zilipaa angani wakati wa hafla hiyo, zikionyesha uwezo wa kijeshi wa taifa hilo la Afrika Mashariki na kuipa hafla hiyo sura ya nguvu na uthabiti wa serikali.
Museveni alikula kiapo na kukabidhiwa nembo zinazoonyesha mamlaka yake kama rais, huku maelfu ya wananchi waliohudhuria sherehe hiyo wakimshangilia.
"Mimi, Yoweri Tibuhaburwa Kaguta Museveni, naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba nitakuwa mwaminifu na mtiifu wa kweli kwa Jamhuri ya Uganda na kwamba nitahifadhi, nitailinda na kuitetea Katiba. Ewe Mungu nisaidie."
Katika hotuba yake, kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 81 amewahimiza raia wa Uganda kuongeza juhudi katika kazi na biashara, akisisitiza umuhimu wa kujenga utajiri wa familia huku akitoa mifano ya watu waliopata mafanikio makubwa kupitia biashara.
Muhula mpya wa saba wa miaka mingine mitano, ndio unaotarajiwa kuwa wa mwisho kwa kiongozi huyo kukaa madarakani.