Marekani itawezaje kuzuia meli za Iran katika Mlango-Bahari wa Hormuz?
Marekani imeanza kuzuia usafiri wa majini wa kuingia na kutoka katika bandari za Iran. Vikosi vya Marekani vinasema vitazuia au kurudisha nyuma meli zinazosafiri kwenda au kutoka pwani ya Iran. Washington inasema meli zinazokuja au kutoka nchi nyingine zitaruhusiwa kupita katika Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya maji ambayo Tehran iliifunga kutokana na mashambulizi ya Marekani na Israel. Marekani itategemea meli zake za majini kudhibiti bandari za Iran, na hivyo kuzuia uwezo wa Tehran kufaidika na mauzo ya mafuta nje ya nchi katika jaribio la kuweka shinikizo kwa nchi hiyo.
Hii inakuja baada ya wapatanishi kutoka pande zote mbili kushindwa kufikia makubaliano ya kukomesha vita, ambavyo vilianza tarehe 28 Februari lakini kwa sasa nchi hizo ziko chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano ya wiki mbili. Trump anataka kuweka shinikizo kwa Iran kwa kulenga shughuli mbili za kiuchumi – moja, ushuru mkubwa ambao Iran ilikuwa inautoza kwa meli ambazo zinapita kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz, pili kuzuia mapato ya Iran kutokana na mauzo ya mafuta. Rais wa Marekani aliiambia Fox News "hatutaiacha Iran ipate pesa kwa kuuza mafuta kwa watu inaowapenda na isiowapenda", akisema lengo ni kuruhusu meli zote kupita kwenye njia hiyo muhimu ya usafirishaji. Iran imejibu kwa kuita kizuizi hicho "uharamia," ikitishia kisasi kwa kushambulia bandari katika mataifa ya Ghuba.
Mwandishi wa habari wa masuala ya usalama wa BBC Frank Gardner anasema kizuizi hicho kinaleta hatari mbili kuu:
- Kitaongeza tena bei ya mafuta na gesi
- Kusitishwa kwa mapigano kutavunjika, vita kamili vinaweza kuzuka tena kati ya Marekani na Iran, pia kuathiri maeneo kama Dubai, Bahrain, Kuwait na Saudi Arabia