Kwa nini Afrika imegawika kuhusu Macky Sall kuiongoza UN
Kwa nini Afrika imegawika kuhusu Macky Sall kuiongoza UN
Burundi ilimteua rais wa zamani wa Senegal Macky Sall kugombea ukatib mkuu wa UN, lakini Afrika imegawika kuhusu kumuunga mkono. Migogoro ya taratibu za AU na siasa za kikanda zimezuia uungwaji mkono wa pamoja.
Burundi mwezi uliopita ilimteua rais wa zamani wa Senegal, Macky Sall, kumrithi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ambaye muhula wake wa pili na wa mwisho unaisha Desemba 31, 2026.
Katika taarifa yake ya maono kwa nafasi hiyo, Sall alisema Umoja wa Mataifa unahitaji kufanyiwa mageuzi, kurahisishwa na kuboreshwa kisasa.
Lakini Senegal ilisema katika noti ya kidiplomasia kwa Umoja wa Afrika (AU) kwamba "haijawahi, katika hatua yoyote, kuidhinisha” ombi hilo, na kwamba pia "haihusiani na hatua husika iliyochukuliwa na Serikali ya Burundi.”
Na matarajio ya Sall ya kupata nafasi ya juu ya Umoja wa Mataifa hayana uungwaji mkono kamili wa AU, ambayo aliiongoza kati ya 2022 na 2023.
Takriban nchi 20 wanachama wa AU zimekataa kumuidhinisha Sall. Nchi muhimu ni pamoja na Afrika Kusini, Algeria, Rwanda, Liberia na Senegal.
Jinsi jaribio lilivyosambaratika
Tarehe 2 Machi, Burundi, ambayo kwa sasa inashikilia nafasi ya mwenyekiti wa AU kwa zamu, iliwasilisha uteuzi wa Sall katika barua kwa rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Kulingana na Taasisi ya Masuala ya Usalama (ISS), taasisi ya utafiti yenye makao Afrika Kusini, "uwasilishaji huo ulifuta mpaka kati ya mpango wa kitaifa na uidhinishaji wa bara.”
ISS ilisema muda wa barua hiyo, iliyosainiwa na Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, "wiki mbili tu baada ya mkutano wa AU, huenda uliunda taswira ya uungwaji mkono rasmi wa AU, na kusababisha mkanganyiko fulani...”
ISS ilibainisha kuwa taratibu za AU zinahitaji wagombea kupitia tathmini rasmi na kamati maalum kabla ya Baraza la Utendaji kuidhinisha, ama kwa makubaliano au kura ya theluthi mbili.
Baada ya maswali na pingamizi kutoka kwa nchi wanachama, Burundi tarehe 26 Machi iliwasilisha tena uteuzi huo chini ya kile kinachoitwa utaratibu wa kimya wa AU (silence procedure), ambao uliwapa wanachama saa 24 pekee kupinga au kuidhinisha.
Utaratibu wa kimya hutumika sana katika taasisi za kimataifa, ukiruhusu maamuzi kupitishwa ikiwa hakuna pingamizi rasmi ndani ya muda uliowekwa.
Kufikia mwisho wa siku ya kazi Machi 27, takriban nchi 20 wanachama wa AU zilivunja ukimya kuhusu rasimu ya uamuzi huo, na hivyo kuzuia kupitishwa kwake.
Nchi zinazopinga zinasema taratibu zilikiukwa
Rwanda, ambayo ilikosoa wazi mchakato huo na kuthibitisha upinzani wake kupitia maafisa wa ngazi ya juu, iliielezea hatua ya Ndayishimiye kama "ukiukwaji mkubwa wa taratibu.”
"Hili lilikuwa kubwa mno kwa nchi nyingi wanachama wa AU, ambazo hazikuweza kukubali amri ya aina hiyo na dharau kutoka kwa mwenyekiti wao. Hivyo ziliamua kuvunja ukimya, kuzuia uamuzi wake na kumkumbusha Rais Ndayishimiye kuwa Umoja wa Afrika unaongozwa na utawala wa sheria,” aliandika Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, kwenye X.
Ujumbe wa Kudumu wa Nigeria kwa AU pia ulivunja ukimya, ukisema kuwa taratibu na kanuni zilizowekwa hazikufuatwa katika kufanya uamuzi huo.
Djiby Sow, mtafiti mwandamizi katika ofisi ya kikanda ya ISS kwa Afrika Magharibi na Sahel, alisema kuwa "AU ina utaratibu uliowekwa katika eneo hili unaoruhusu tathmini ya kina ya wagombea.”
"Na katika tukio hili, utaratibu wa kimya haukuruhusu majadiliano kuhusu suala muhimu sana kama ugombea wa nafasi ya Katibu Mkuu,” Sow aliiambia DW.
Katika barua kwa Tume ya AU, Nigeria ilisema Afrika inapaswa kujizuia kugombea nafasi ya Katibu Mkuu, ikisema ni zamu ya Amerika ya Kusini na Karibiani kulingana na "kanuni ya muda mrefu ya mzunguko wa mabara katika uteuzi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.”
Nini kinafuata?
Hata bila uidhinishaji wa AU, Sall bado ni mgombea wa nafasi ya mkuu wa Umoja wa Mataifa, na nchi wanachama ziko huru kumpigia kura kwa misingi ya binafsi.
Sall anaungana na wagombea wengine watatu katika kinyang'anyiro cha kumrithi Guterres kuanzia Januari 1, 2027: Rebeca Grynspan, aliyekuwa makamu wa rais wa Costa Rica; Rafael Grossi, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA); na rais wa zamani wa Chile, Michelle Bachelet.
Wamepangwa kufanyiwa mahojiano na nchi wanachama katika nusu ya pili ya Aprili.