KIPIMO CHA UWAJIBIKAJI WA SEKTA YA AFYA NI KURIDHIKA KWA WANANCHI – DKT. MAGEMBE
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, amewataka viongozi na watumishi wa sekta ya afya nchini kufanya kazi kwa weledi, uwajibikaji na ufanisi, akisisitiza kuwa kipimo kikuu cha mafanikio ya sekta hiyo ni kiwango cha kuridhika kwa wananchi wanaopokea huduma za afya.
Akizungumza leo Julai 1, 2026, katika Ofisi ndogo za Wizara ya Afya zilizopo katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dar es Salaam, mara baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Magembe amesema sekta ya afya inahusu maisha ya watu, hivyo kila mtumishi anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa umakini, kujituma na kuwajibika.
Amesema huduma zinazotolewa zinapaswa kupimwa kwa kiwango cha kuridhika kwa wananchi, akibainisha kuwa uhai wa binadamu hauwezi kusubiri, hivyo watumishi wanapaswa kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha huduma wanazotoa zinakidhi matarajio ya wananchi.
Dkt. Magembe amewataka viongozi wa sekta ya afya kusimamia ipasavyo watumishi walio chini yao ili kuhakikisha taaluma na utaalamu wao vinaendelea kuboresha utoaji wa huduma. Amesisitiza kuwa utaalamu wa kila mtumishi unapaswa kuonekana kupitia manufaa yanayopatikana kwa wananchi.
Aidha, amewahimiza viongozi kuendelea kuibeba ajenda ya Serikali ya kuimarisha uzalishaji wa bidhaa za afya nchini, kuongeza uwekezaji katika viwanda vya ndani, pamoja na kuhamasisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote na kuboresha ubora wa huduma za afya.
Dkt. Magembe amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani aliyompa kupitia uteuzi huo, pamoja na Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, kwa ushirikiano anaouendelea kutoa katika kuimarisha sekta ya afya.
Aidha, ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na mfumo wa timu, akieleza kuwa maono ya Serikali ya kuendelea kuboresha huduma za afya yatafanikiwa kupitia umoja, mshikamano na uwajibikaji wa viongozi na watumishi wote wa sekta ya afya.